
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amewataka wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi kutofumbia macho vitendo vya uhalifu, badala yake watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua stahiki zichukuliwe.
Wito huo umetolewa leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Tarafani, Mbalizi, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni ya “Ongea na Kamanda” inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kudumisha amani na usalama.
Katika mkutano huo, Kamanda Kuzaga amewataka wananchi kukemea vitendo vya uhalifu katika jamii, huku akisisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto ili wakue katika misingi ya maadili mema na kujiepusha na vitendo vya uhalifu.
Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazoweza kusababisha mafuriko, akihimiza kuendelea kufanya usafi wa mazingira na kuondoa taka ngumu kwenye mitaro ili kuruhusu maji kutiririka kwa urahisi.
Pia amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuongeza uangalizi kwa watoto ili kuwakinga dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kuzaga amewakumbusha wananchi wanaomiliki silaha bila vibali halali kuzisalimisha katika vituo vya Polisi, ofisi za Serikali au kwa watendaji wa kata kabla ya Oktoba 31, 2026.
Amesema baada ya muda huo, operesheni itafanyika na yeyote atakayebainika kumiliki silaha kinyume cha sheria atachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Anganile Amosi, mkazi wa Mbalizi, ameipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zake za kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani.

Hata hivyo, ameiomba Serikali kuboresha barabara ya mchepuko ili iweze kupitika kwa urahisi, hasa kwa magari madogo, hatua ambayo itasaidia kurahisisha usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.

Leave a Reply