Mwandishi Wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Fadhil Nkurlu, ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) kuhakikisha huduma za maji na umeme zinawafikia wananchi wa Mtaa wa Saeni na Karabaka, Kata ya Misugusugu, ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

Agizo hilo amelitoa hivi karibuni katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Misugusugu, ambapo alipata fursa ya kusikiliza na kupokea kero pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa eneo hilo.

Akijibu kuhusu upatikanaji wa huduma za maji na umeme, wawakilishi wa TANESCO na DAWASA walimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa ifikapo mwezi Desemba wananchi wataanza kupata huduma hizo. Walisema miundombinu muhimu tayari imewekwa na kilichobaki ni hatua chache za ukamilishaji, huku fedha kwa ajili ya utekelezaji zikiwa zimepatikana.

Katika mkutano huo, wananchi pia waliwasilisha malalamiko kuhusu uchafuzi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wamiliki wa viwanda vilivyopo katika maeneo yao.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Nkurlu alisema ofisi yake ipo katika hatua za kufanya mazungumzo na wamiliki wa viwanda vyote vinavyohusika ili kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Alisema mikakati hiyo itajumuisha kudhibiti utiririshaji wa maji taka katika maeneo ya makazi ya wananchi ili kulinda afya za wakazi na mazingira kwa ujumla.

Changamoto nyingine zilizowasilishwa na wananchi ni pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi na soko. Akizungumzia hoja hizo, Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi wa Kata ya Misugusugu kupendekeza maeneo yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo ili kurahisisha utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu, Sarah Uledi, alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutembelea kata hiyo, kusikiliza kero za wananchi na kutoa ufafanuzi kuhusu changamoto mbalimbali.

Alisema anaamini ziara hiyo imekuwa faraja kwa wananchi na imesaidia kutoa majibu ya masuala yaliyokuwa yakiwasumbua kwa muda mrefu, hususan upatikanaji wa huduma za maji na umeme.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Moses Magongwa, Mtendaji wa Kata, watendaji wa mitaa, wenyeviti wa serikali za mitaa na wataalamu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Posted in

Leave a Reply