Na Iddy Mziray – Songea, Ruvuma

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Ruvuma, ACP Ramia Mganga, akiambatana na Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Songea, ASP Melinda Mgumba, amekutana na wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mwengemshindo, Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, na kuwataka kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama katika jamii.

Viongozi hao wa Polisi Jamii walitembelea wajumbe hao wakati wa mkutano wao wa mafunzo, ambapo ACP Ramia alieleza umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi katika kuzuia uhalifu, kulinda mali na kudumisha amani katika maeneo yao.

Aidha, ACP Ramia ametangaza kuanza kwa operesheni ya kurejesha silaha zinazomilikiwa na wananchi bila vibali halali, akiwataka wote wenye silaha hizo kuzirejesha kwa hiari kwa Jeshi la Polisi.

Amesema Serikali imetoa fursa kwa watu wanaomiliki silaha bila vibali halali kuzikabidhi kwa hiari, huku akieleza kuwa muda wa zoezi hilo unaishia Oktoba 30, 2026.

“Tunatoa wito kwa wananchi wote wa Ruvuma na Songea kwa ujumla wanaomiliki silaha bila kibali kuziwasilisha Polisi. Hutashitakiwa, na kama unataka kumiliki silaha kihalali, njoo na silaha yako kituo cha Polisi tutakupa taratibu zote za kumilikishwa kihalali,” amesema ACP Ramia Mganga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Songea, ASP Melinda Mgumba, amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto, hasa katika kipindi cha msimu wa mvua, ambapo maji mengi na mafuriko vinaweza kuhatarisha maisha yao.

ASP Melinda amewataka wazazi kutowaacha watoto wakicheza kwenye madimbwi, mito na maeneo mengine hatarishi wakati wa mvua kubwa, ili kuepusha ajali na maafa yanayoweza kutokea.

Aidha, amewahimiza wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la Polisi, akisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuzuia vitendo vya uhalifu na kuwabaini wanaohusika.

Amesema wananchi wanaokutana na silaha zilizotelekezwa, wanaotaka kurejesha silaha kwa hiari au wenye taarifa nyingine za uhalifu wanapaswa kuwasiliana na Polisi Jamii kupitia namba rasmi za mawasiliano au kufika katika kituo cha Polisi kilicho karibu.

Vilevile, amewataka wananchi kuhakikisha taarifa wanazozitoa kuhusu uhalifu na wahalifu ni za kweli, akionya dhidi ya kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kumchafua au kumsingizia mtu kutokana na chuki binafsi.

Wajumbe wa CCM Kata ya Mwengemshindo wameishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu hiyo na kuahidi kushirikiana nalo katika kuimarisha amani, kuzuia uhalifu na kuwa mabalozi wa usalama katika kata yao.

Posted in

Leave a Reply