
Na Mwandishi Wetu
Miili ya askari watatu wa Jeshi la Polisi waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Magole, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, inaagwa leo katika viwanja vya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
Askari hao ni miongoni mwa watu wanne waliofariki katika ajali iliyotokea jioni ya Oktoba 8, 2026, ikihusisha gari la Polisi lililokuwa likisafiri kutoka Morogoro kuelekea Turiani na malori mawili aina ya Scania.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, ajali hiyo ilihusisha gari la Polisi lenye namba za usajili PT 5361 GMW, lori lenye namba T 309 EMK na trela T 424 DUM, pamoja na lori jingine lenye namba T 755 AJS na trela T 897 AJJ.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wanne na kujeruhi wengine saba, ambao walikimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Kamanda Kantimbo amesema uchunguzi ulikuwa ukiendelea kubaini chanzo na mazingira yaliyosababisha magari hayo kugongana.
Shughuli za kuwaaga askari hao zinatarajiwa kufanyika kuanzia asubuhi hadi mchana wa leo, Oktoba 10, 2026. Zinatarajiwa kuhudhuriwa na wananchi, askari na viongozi wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu na Mkoa wa Morogoro.
Kuagwa kwa askari hao ni sehemu ya taratibu za mwisho za kuwapa heshima watumishi hao waliopoteza maisha katika ajali hiyo wakiwa safarini.
Leave a Reply