
Na Mwandishi Wetu
Serikali imezitaka taasisi na wadau wa sekta ya posta nchini kuimarisha mifumo ya kidijitali ya kufuatilia nyaraka na vifurushi ili kuwawezesha wateja kupata taarifa sahihi kuhusu mizigo yao katika hatua zote za usafirishaji.
Aidha, wadau hao wametakiwa kuboresha huduma za posta ili ziendane na mahitaji ya uchumi wa kidijitali, hususan ukuaji wa biashara za mtandaoni.
Wito huo umetolewa jana na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Dk. Switbert Mkama, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Alisema ukuaji wa biashara za mtandaoni unahitaji huduma za posta zilizo za haraka, salama na nafuu.
Aliongeza kuwa mtandao wa posta uliounganishwa vizuri utasaidia wafanyabiashara wadogo kufikia masoko mapana, kuongeza fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, aliitaka Shirika la Posta Tanzania kuboresha huduma zake ili ziwafikie wananchi wa vijijini, maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara pamoja na watu wenye mahitaji maalumu.
Kwa upande wake, Kaimu Posta Masta Mkuu, Ferdinard Kabyemela, alisema wanafunzi 1,333 kutoka shule za msingi na sekondari walishiriki shindano la kimataifa la uandishi wa barua. Kati yao, wavulana walikuwa 508 na wasichana 825.
Alisema shindano hilo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza utamaduni wa kuandika barua na kuwajengea vijana uwezo wa kueleza na kuwasilisha mawazo yao, licha ya mabadiliko yanayotokana na matumizi ya teknolojia katika mawasiliano.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Peter Mwasalyanda, alisema mamlaka hiyo itaendelea kusimamia sekta ya posta na kulinda haki za watumiaji wa huduma hizo.
Aliwataka wananchi kuripoti changamoto wanazokutana nazo kwa watoa huduma za posta wenye leseni ili ziweze kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Maadhimisho hayo yalifanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Mtandao Mmoja wa Posta, Fursa Zisizo na Ukomo.”
Leave a Reply