
Na Iddy Mziray, Songea
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Marco Chilya, amezindua programu ya “Ongea na Kamanda” kwa kukutana na wananchi wa Kata ya Mwenge-Mshindindo, Mtaa wa Mwanamonga, Manispaa ya Songea, kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii katika kudumisha amani na usalama.
Kupitia programu hiyo, Chilya alisikiliza malalamiko, maoni na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, huku akitoa ufafanuzi na maelekezo kuhusu namna ya kuzitatua.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu uhalifu na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama katika maeneo yao.
Akizungumza na wananchi hao, Chilya alisema mawasiliano ya karibu kati ya Jeshi la Polisi na jamii ni nyenzo muhimu katika kutatua changamoto za kiusalama, kuzuia uhalifu na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata hiyo, Osmundi Kapinga, alisema yeye pamoja na wananchi wa Mwenge-Mshindindo wameipokea programu hiyo kwa mtazamo chanya kwa kuwa inawapa fursa ya kuwasilisha kero na changamoto zao moja kwa moja kwa uongozi wa Jeshi la Polisi.

Kapinga aliipongeza Jeshi la Polisi kwa kuanzisha utaratibu huo wa mawasiliano, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya aina hiyo ili wananchi wapate ufafanuzi wa masuala yanayowakabili na kuimarisha uhusiano wao na Jeshi la Polisi.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Ruvuma, ACP Ramia Mganga, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Songea, maofisa wa Polisi Kata, watendaji wa kata, diwani na wananchi wa Kata ya Mwenge-Mshindindo, Mtaa wa Mwanamonga.

Leave a Reply