
Na Andrea Mlwafu
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Temeke, limetambua watumishi watatu kutokana na utendaji wao mzuri kazini, katika hatua inayolenga kuhamasisha uwajibikaji, kujituma na kuboresha huduma kwa wateja.
Watumishi hao walitambuliwa katika hafla ya kuhitimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 iliyofanyika katika ofisi za TANESCO Mkoa wa Temeke, zilizopo Kurasini, Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Nickson Babu, aliwataka watumishi kuongeza juhudi katika kutekeleza majukumu yao. Alisisitiza umuhimu wa uzalendo, nidhamu na uwajibikaji katika kuboresha utendaji wa shirika hilo.
Babu alisema kuwa watumishi wanapaswa kwenda zaidi ya kutekeleza majukumu yao ya kawaida kwa kuhakikisha wanatoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wateja.
Watumishi waliotambuliwa ni Hussein Mchomvu kutoka Idara ya Ufundi, Ofisi ya Mkoa wa Temeke; Mustapha Hamza kutoka Idara ya Uhusiano na Huduma kwa Wateja, Ofisi ya Wilaya ya Mbagala; na Angela Kalambo kutoka idara hiyo katika Ofisi ya Wilaya ya Yombo.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, watumishi hao waliushukuru uongozi wa shirika hilo kwa kutambua mchango wao.

Walisema kuwa hatua hiyo imewapa motisha ya kuendelea kuongeza juhudi na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2026, iliyobeba kaulimbiu “Mbele Zaidi Kihuduma,” TANESCO Mkoa wa Temeke iliendesha shughuli mbalimbali, zikiwemo usafi wa mazingira, kikao kazi na wadau wa nishati, pamoja na vikao vya watumishi vilivyolenga kuweka mikakati ya kuboresha huduma.
Utambuzi huo ni sehemu ya juhudi za TANESCO Mkoa wa Temeke za kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji miongoni mwa watumishi na kusisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora kwa wateja.


Leave a Reply