
Na Andrea Mlwafu
Serikali imetakiwa kuimarisha mitaala ya elimu kwa kusisitiza ujuzi wa vitendo ili kuwawezesha vijana kutumia maarifa wanayopata shuleni na vyuoni kuanzisha shughuli za kiuchumi badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa pekee.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya St. Mary’s Duluti, Matei Malya, wakati wa mahafali ya 17 ya Kidato cha Nne yaliyofanyika shuleni hapo, mkoani Arusha.

Malya alisema maboresho ya mitaala yanapaswa kuambatana na usimamizi madhubuti wa utekelezaji wake, hususan katika masomo ya amali, ili wahitimu wa shule za sekondari na vyuo vya kati waweze kubuni shughuli za kiuchumi na kutumia fursa zilizopo katika jamii.
Alisema ubunifu uliooneshwa na wanafunzi wa shule hiyo unaashiria kuwa elimu inaweza kuwa msingi wa ujasiriamali iwapo wanafunzi watawezeshwa kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya maisha na soko la ajira.
Aliongeza kuwa kuwaandaa vijana kujitegemea kunahitaji ushirikiano kati ya Serikali, wazazi, walezi na wadau wa elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa pamoja na ujuzi wa vitendo.
Malya aliwataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa kuwapatia watoto mahitaji muhimu ya shule, yakiwemo sare na vitabu, pamoja na kutimiza wajibu wa kulipa ada pale inapohitajika. Pia aliwasisitiza kufuatilia maendeleo ya watoto wao kitaaluma na kitabia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Mary’s Duluti, Bro. Protas Mangu, alisema shule hiyo imekuwa ikiwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri kupitia masomo ya vitendo na shughuli zinazochochea ubunifu.

Alisema lengo ni kuhakikisha wahitimu wanatumia maarifa na ujuzi walioupata kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazowawezesha kujitegemea katika maeneo watakayoishi baada ya kumaliza masomo.
Aidha, aliwataka wahitimu kudumisha nidhamu, kujiamini na kuwajibika ili kufikia malengo yao. Pia aliwahimiza kuepuka ulevi, uvivu na matumizi yasiyofaa ya mitandao ya kijamii.
Alisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji bidii, subira na uadilifu, huku akiwataka vijana kuepuka njia zisizo halali katika kutafuta maisha bora.
Naye Padre Adolf Msoka aliwahimiza wahitimu kuzingatia mafundisho ya dini, kudumisha maadili mema na kutumia maarifa waliyopata shuleni kwa manufaa yao na ya jamii kwa ujumla.
Mahafali hayo yameweka msisitizo katika nafasi ya elimu ya vitendo, ubunifu na maadili katika kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za maisha na kutumia fursa za kujitegemea baada ya kuhitimu.

Leave a Reply