Na Andrea Mlwafu

Serikali imezitaka mamlaka za Dar es Salaam kuimarisha usimamizi wa mazingira na kuchukua hatua za kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, wakati wa ziara ya kukagua hali ya mazingira katika Mto Ng’ombe, Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Masauni alisema taasisi na mamlaka zinazohusika zinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji bila kusubiri maelekezo kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu. Alisisitiza kuwa Dar es Salaam ni taswira ya nchi, hivyo viongozi katika ngazi zote wana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanalindwa.

Alionya kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais haitavumilia uzembe katika utekelezaji wa majukumu ya utunzaji wa mazingira. Aidha, alisema changamoto za makazi katika baadhi ya maeneo hazipaswi kuwa kikwazo katika kudhibiti utupaji holela wa taka.

Waziri huyo alieleza kuwa taka zinaweza kuwa chanzo cha mapato na ajira kwa wananchi endapo zitachakatwa na kuongezewa thamani. Alizitaka mamlaka kuweka mifumo inayowezesha matumizi upya ya taka ili kupunguza uchafuzi na kulinda afya za wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, alisema wilaya hiyo inaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira.

Alisema wakazi wanaoishi karibu na Mto Ng’ombe wameelekezwa kuhama katika maeneo hayo ili kujikinga na madhara yanayoweza kutokea wakati wa mvua, huku zoezi la kubomoa nyumba zilizopo katika maeneo husika likiwa limeanza.

Mtambule alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi ni muhimu katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kupunguza hatari zinazoweza kusababishwa na mvua.

Posted in

Leave a Reply