Na Mwandishi Wetu

Mwenyekiti wa Kamati ya Maji katika Kata za Malya na Lyoma (Mwamama), Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, Stiven Muhina (47), amefariki dunia katika ajali ya pikipiki, siku chache baada ya kuwasilisha kero ya maji mbele ya Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, amesema ajali hiyo ilitokea Oktoba 15, 2026, saa 9:05 alasiri, katika Kijiji na Kata ya Malya, wilayani Kwimba.

Amesema ajali hiyo ilihusisha pikipiki aina ya Skymark, yenye namba za usajili MC 647 DCM, iliyokuwa ikiendeshwa na Muhina kutoka Malya Kati kuelekea eneo la Mjini A. Pikipiki hiyo iligonga mti uliokuwa kando ya barabara na kusababisha kifo chake papo hapo.

Kwa mujibu wa Mutafungwa, uchunguzi wa awali unaangalia uwezekano wa mwendokasi na matumizi ya pombe kuchangia ajali hiyo. Amesema marehemu pia hakuwa amevaa kofia ngumu wakati wa ajali.

Mwili wa Muhina umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba kwa ajili ya taratibu za kisheria kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa mazishi.

Kifo chake kimetokea siku chache baada ya kuwasilisha changamoto ya upatikanaji wa maji katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Malya, mbele ya Makonda aliyekuwa katika ziara mkoani Mwanza.

Makonda ameeleza kusikitishwa na taarifa za kifo cha mwenyekiti huyo.

Mutafungwa amewataka watumiaji wa barabara kuzingatia kanuni za usalama barabarani, ikiwamo matumizi ya kofia ngumu kwa waendesha pikipiki.

Posted in

Leave a Reply