Na Abel Mwakingwe

Tanzania imepiga hatua katika biashara ya kaboni baada ya miradi sita kufikia hatua ya kuzalisha krediti za kaboni, huku Serikali ikiendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa miradi hiyo kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kijani na kuhakikisha wananchi wananufaika.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alisema hayo hivi karibuni jijini Kigali, Rwanda, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika wa mwaka 2026.

Masauni alisema hatua hiyo inaonesha maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania katika kujenga soko la kaboni linalozingatia uwazi, uadilifu na uhifadhi wa mazingira.

Alieleza kuwa katika kikao cha hivi karibuni cha Kamati ya Taifa ya Kutathmini Miradi ya Kaboni, miradi minne inayohusisha nishati safi ya kupikia na manufaa ya kijamii iliidhinishwa baada ya kufikia hatua ya ukomavu.

Alisema Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya kisera na kitaasisi inayosimamia biashara ya kaboni, ikiwemo kuanzishwa kwa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kupitia marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Masauni, kituo hicho kina jukumu la kusajili miradi ya kaboni, kusimamia upimaji na uhakiki wa matokeo yake, pamoja na kuzuia matokeo ya miradi kuhesabiwa zaidi ya mara moja.

Aidha, alizitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji na taasisi za kifedha ili kupata mitaji ya muda mrefu, kuongeza utekelezaji wa miradi na kuhakikisha wananchi wananufaika na mapato yatokanayo na biashara hiyo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NCMC, Kathryn Kigaraba, alisema mkutano huo ni fursa kwa wadau kujadili namna ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na kujenga soko la kaboni lenye uaminifu na manufaa kwa jamii.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Semesi, alisema baraza hilo litaendelea kushirikiana na NCMC katika kusimamia miradi ya kaboni ili kulinda mazingira na kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi hiyo.

Posted in

Leave a Reply