Na Mwandishi Wetu

MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, kuhakikisha mkandarasi anayetekeleza mradi wa upanuzi wa barabara ya Tanzania na Zambia (TANZAM) katikati ya Jiji la Mbeya anafungua barabara za mitaa alizozifunga ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao.

Ndejembi alitoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, ambapo alieleza kutoridhishwa na mwenendo wa kazi zinazotekelezwa na mkandarasi huyo, akisema zimekuwa kero kwa wananchi, hususan wajasiriamali.

Alisema mkandarasi amefukua barabara yenye urefu wa kilomita 29 bila kuwa na utayari wa kutekeleza ujenzi katika maeneo yote kwa wakati mmoja, hali iliyosababisha wananchi kukabiliwa na vumbi na mafuriko.

Aidha, alisema kufungwa kwa barabara hizo kumeongeza gharama za usafiri kwa wananchi, ambao sasa wanalazimika kutembea kwa miguu kuvuka baadhi ya maeneo badala ya kutumia vyombo vya usafiri kama ilivyokuwa awali.

“Naomba niwaambie wananchi wa Jiji la Mbeya kwamba sijaridhishwa na kinachofanyika kwenye mradi huu. Nitapita kesho ninapokwenda Mbarali, nataka nimkute mkandarasi akiwa anarekebisha maeneo yote aliyoziba,” alisema Ndejembi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, alisema ana wasiwasi kuhusu usahihi wa taarifa zilizowasilishwa na mkandarasi wakati wa mchakato wa kuomba zabuni, akieleza kuwa huenda baadhi yake hazikuwa sahihi na zikachangia kampuni hiyo kupata zabuni.

Alisema uwezo wa kifedha ni miongoni mwa vigezo vinavyotumika katika kumpata mkandarasi, akibainisha kuwa kampuni ya CHICO ilionesha kuwa na Sh bilioni 20 katika akaunti yake, jambo lililochangia kuaminiwa wakati wa mchakato wa zabuni.

Posted in

Leave a Reply