
Na Majura Mathias
Mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi ya Umma yamefungua fursa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia zabuni za Serikali, hatua inayolenga kuongeza kipato, kukuza ajira na kuchochea maendeleo katika maeneo yao.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Japhari Kubecha, alipokuwa akizungumza na wanufaika wa vikundi vinavyotekeleza shughuli za usafi wa mazingira na barabara chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya usafi iliyofanyika katika ofisi za TARURA Wilaya ya Gairo, Kata ya Ukwamani.
Kubecha amesema mabadiliko hayo yanawezesha wananchi, hususan vijana, kutumia fursa zinazotokana na manunuzi ya umma kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Ramadhani Kimwaga, amesema utekelezaji wa mpango huo unalenga kutumia fursa zinazotokana na Sheria ya Manunuzi ya Umma, ambapo vikundi vya vijana vilivyosajiliwa katika Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Kielektroniki (NeST) vinaweza kushiriki katika zabuni mbalimbali za Serikali.
Amesema ushiriki huo unatoa fursa kwa vijana kujiongezea kipato, kukuza shughuli zao za kiuchumi na kujenga uwezo wa kujitegemea.
Aidha, Kimwaga amesema zoezi la usafi wa mazingira ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa, ikiwemo mafuriko. Ameeleza kuwa usafishaji wa mitaro na maeneo mengine ya kupitisha maji utasaidia kupunguza uwezekano wa maji kuziba njia na kuathiri makazi pamoja na miundombinu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Sharifa Nabalang’anya, amesema kukabidhiwa kwa vifaa hivyo ni hatua ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusu kuwawezesha wananchi, hususan makundi maalumu, kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na manunuzi ya umma.

Amesema hatua hiyo inalenga kukuza ajira, kuongeza kipato na kuwasaidia wananchi kuanzisha na kuendeleza shughuli endelevu za kiuchumi.
Hafla hiyo imehusisha ugawaji wa vifaa vya usafi kwa vikundi 14 kutoka kata 12 kati ya kata 18 za Halmashauri ya Wilaya ya Gairo. Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usafi wa mazingira, kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi na kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa.


Leave a Reply