
Na Majura Mathias, Gairo
Maandalizi ya Maonesho ya Gairo Kilimo Biashara Expo 2026, msimu wa tano, yamefikia hatua za mwisho kufuatia kukamilika kwa hatua mbalimbali za maandalizi ya tukio hilo linalolenga kuwaunganisha wadau wa sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuongeza tija na kuimarisha fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Maonesho hayo yanatarajiwa kuanza rasmi Oktoba 30, 2026, katika Viwanja vya Gulio la Chakwale. Ufunguzi rasmi utafanyika Jumamosi, Oktoba 31, 2026, katika Viwanja vya Gulio la Rubeho, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Mifugo, Mhe. Ng’wasi Kamani.
Maonesho hayo yatawakutanisha wakulima, wafugaji, wauzaji na wasambazaji wa pembejeo za kilimo, viuatilifu na dawa za mifugo, taasisi za fedha pamoja na wadau wengine muhimu katika mnyororo wa thamani wa sekta hizo.
Akizungumza katika kikao cha wataalamu wa sekta hizo kilichofanyika Oktoba 26, 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maonesho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Japhari Kubecha, aliwataka wataalamu kuhakikisha hatua zote muhimu za maandalizi zinakamilishwa kwa wakati na kuzingatia viwango vinavyotakiwa ili kufanikisha tukio hilo.
Kubecha alisema maonesho hayo yanapaswa kuwa jukwaa la kuwaunganisha wadau, kubadilishana maarifa na teknolojia, kutangaza fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano katika sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji, pamoja na kuboresha kipato na maisha ya wananchi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya, Jeremiah Mapogo; Afisa Tarafa ya Gairo, Chifu Mukama; Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi; wataalamu wa kilimo na mifugo; Afisa Habari; Afisa Ushirika pamoja na wataalamu wengine kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, maonesho hayo yataendelea hadi Novemba 3, 2026, ambapo yatafungwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Gairo ‘A’.
Maonesho ya msimu wa tano yanatarajiwa kutoa fursa kwa wadau kujifunza mbinu bora za uzalishaji, kupata huduma na taarifa za kitaalamu, pamoja na kujenga mitandao ya kibiashara itakayochochea maendeleo ya sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi wilayani Gairo na maeneo mengine.

Leave a Reply