Na Happy Milion

Zaidi ya wananchi 9,000 kutoka vijiji 32 katika kata sita za Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, wananufaika na mradi wa umeme wa upepo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 3.9, unaotekelezwa katika Kijiji cha Usokami.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka viongozi wa vijiji vinavyozunguka mradi huo kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu yake ili kuhakikisha inaendelea kutoa huduma ya umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza leo alipotembelea mradi huo, James alisema wananchi wanapaswa kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme kuanzisha na kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

“Uwepo wa umeme wa uhakika unaweza kuwa chachu ya kukuza shughuli za kiuchumi, kuongeza kipato cha kaya na kuboresha maisha ya wananchi. Hivyo, ni muhimu kwa jamii kushirikiana katika kuutunza mradi huu,” alisema James.

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Mwenge Hydro Power Ltd, Deogratius Massawe, alisema kampuni hiyo inalenga kuwapatia wananchi huduma ya umeme ya uhakika na kwa gharama nafuu ili kuwawezesha kupanua shughuli za uzalishaji na biashara.

Alisema upatikanaji wa nishati hiyo unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi na kuchochea maendeleo katika jamii zinazozunguka mradi huo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wanufaika, Michael Mahenge alisema mradi huo umeleta mabadiliko chanya kwa kurahisisha shughuli mbalimbali ambazo awali zilikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme.

Alisema upatikanaji wa umeme umewawezesha wananchi kusaga mahindi ndani ya kijiji chao, hivyo kupunguza usumbufu na gharama za kusafirisha mahindi kwenda maeneo mengine. Aidha, fursa hiyo imefungua milango ya kuongeza kipato kupitia shughuli ndogo ndogo za uzalishaji.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 50 ni sehemu ya uwekezaji katika sekta ya nishati unaolenga kuboresha upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayohudumiwa.

Posted in

Leave a Reply