Na Andrea Mlwafu

Jeshi la Polisi wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, limewataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Uuguzi na Ukunga Same kutumia vizuri muda wao kwa kujikita katika masomo na shughuli zenye tija, huku likiwaonya dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Same, SSP Tom Obonyo, wakati wa operesheni ya Ongea na Kamanda, inayolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu usalama na namna ya kuzuia uhalifu.

Obonyo amewahimiza wanachuo hao kuzingatia malengo yaliyowapeleka chuoni, akisisitiza kuwa elimu wanayoipata ni msingi wa kutimiza ndoto zao, kujenga maisha bora na kulitumikia taifa.

Amewaonya pia dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, ikiwemo mirungi, akieleza kuwa tabia hiyo inaweza kuathiri afya zao, maendeleo ya kitaaluma na mustakabali wa maisha yao. Ameongeza kuwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uhalifu watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, amewataka wanafunzi kutambua na kuthamini juhudi za wazazi na walezi wanaogharamia elimu yao kwa kutumia muda wao vizuri, kuepuka uzururaji na kujikita katika masomo ili kufikia malengo yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, SSP Asia Matauka, amewataka wanachuo hao kujiepusha na vitendo vya ukatili, kuheshimiana na kutatua changamoto zinazowakabili kwa njia zinazokubalika kisheria.

Matauka amesisitiza umuhimu wa kuwa makini katika mahusiano, huku akiwahimiza wanafunzi kuepuka imani za kishirikina zinazoweza kuchochea vitendo vya ukatili na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapokabiliwa na changamoto zinazohitaji msaada.

Naye Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Lazaro Mwanyasi, amewahimiza wanafunzi kuheshimu sheria na kanuni za chuo, kusoma kwa bidii na kudumisha uzalendo ili wawe wataalamu wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao, wanachuo hao wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu waliyoipata na kuahidi kuzingatia maadili, nidhamu na uzalendo, huku wakijiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha masomo yao na maisha yao ya baadaye.

Posted in

Leave a Reply