Na Neema Patrick

Madereva wanaosafirisha kemikali nchini wamepewa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usafirishaji wa kemikali na bidhaa hatarishi ili kulinda maisha ya watu, mazingira na mali, pamoja na kuzuia ajali zinazoweza kusababishwa na uzembe au ukiukwaji wa taratibu za usalama.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Danstan Mkapa, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali yaliyowakutanisha madereva wa malori yanayosafirisha bidhaa hizo.

Mkapa alisema kuwa licha ya kemikali kuwa na umuhimu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, usafirishaji wake unahitaji umakini mkubwa na uzingatiaji wa sheria na kanuni zinazotumika ili kuzuia ajali, uchafuzi wa mazingira na madhara mengine yanayoweza kutokea wakati wa safari.

Alisisitiza kuwa madereva wanapaswa kuhakikisha magari wanayotumia yako katika hali nzuri, mizigo imefungwa na kuhifadhiwa kwa usalama, na nyaraka zote zinazotakiwa kisheria zinakuwepo kabla ya kuanza safari.

“Kuzingatia sheria na kanuni si jambo la hiari. Ni wajibu wa kila dereva na mmiliki wa chombo cha usafiri kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa unafanyika kwa usalama ili kulinda maisha ya watu, mazingira na mali,” alisema Mkapa.

Aidha, aliwataka madereva kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutoa taarifa wanapobaini changamoto zinazoweza kuhatarisha usalama wakati wa kusafirisha kemikali na bidhaa nyingine zinazohitaji uangalizi maalumu.

Aliongeza kuwa madereva wanapaswa kuwa mabalozi wa usalama kwa wenzao kwa kuzingatia mafunzo wanayopata na kuyatumia katika shughuli zao za kila siku.

Wakizungumzia manufaa ya mafunzo hayo, baadhi ya madereva walioshiriki walisema yamewaongezea uelewa kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha kemikali na bidhaa nyingine hatarishi zinasafirishwa kwa usalama, bila kuhatarisha jamii na mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya madereva wenzake, Shabani Mavengelo alisema mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa umuhimu wa kuwa na nyaraka sahihi za usafirishaji, kufahamu aina ya mzigo anaousafirisha na kufuata taratibu za dharura endapo ajali itatokea.

Alisema pia wamepata elimu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kinga binafsi na hatua za kuzingatia ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa usafirishaji.

Alifafanua kuwa usafirishaji salama wa kemikali hauishii katika kufikisha mzigo mahali unapokwenda, bali unahusisha maandalizi ya safari, ukaguzi wa gari, ufungaji na uhifadhi salama wa mzigo, pamoja na kuzingatia sheria za usalama barabarani.

“Tumejifunza mambo mengi ambayo hatukuwa tunayafahamu kwa kina. Sasa tunaelewa wajibu wetu katika kulinda maisha ya wananchi, mazingira na mali wakati wa kusafirisha bidhaa mbalimbali,” alisema Mavengelo.

Madereva hao waliishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo na kuiomba iendelee kuyaendesha mara kwa mara ili kuwafikia madereva wengi zaidi nchini.

Walisema kuendelezwa kwa mafunzo hayo kutasaidia kuongeza uelewa kuhusu usafirishaji salama wa kemikali, kuimarisha uzingatiaji wa sheria na taratibu, na kupunguza ajali pamoja na madhara yanayoweza kusababishwa na usafirishaji usio salama.

Posted in

Leave a Reply