
Na Mwandishi Wetu
Watu wawili, akiwamo Diwani wa Kata ya Kinyangiri, Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wamepanda kugongana na gari aina ya Toyota Harrier katika barabara ya Singida–Veta, mjini Singida.
Ajali hiyo imetokea jana usiku katika eneo la Veta, Kata ya Utemini, Manispaa ya Singida, na kusababisha vifo vya watu hao wawili pamoja na uharibifu wa vyombo vya usafiri vilivyohusika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Matride Kuyeto, ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 757 EBJ, lililokuwa likiendeshwa na Athumani Mkalimoto (42), mfanyakazi wa SUWASA na mkazi wa Mwaja.
Gari hilo liligongana na pikipiki aina ya Haojue yenye namba za usajili MC 131 FNY, iliyokuwa ikiendeshwa na Selemani Athumani Hamis (27), mkazi wa Veta.
Kamanda Kuyeto amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Selemani Athumani Hamis, aliyekuwa akiendesha pikipiki hiyo, na Athumani Hamis (53), Diwani wa Kata ya Kinyangiri, Wilaya ya Mkalama, aliyekuwa abiria kwenye pikipiki hiyo.
Leave a Reply