Na Mwandishi Wetu, Katavi
Wakulima mkoani Katavi wametakiwa kuendelea na shughuli za kilimo licha ya kushuka kwa bei za baadhi ya mazao, hali iliyosababisha baadhi yao kushindwa kurejesha mikopo ya pembejeo na wengine kukabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi wakati alipotembelea na kukagua mabanda mbalimbali yanayohusika na shughuli za kilimo katika maonesho ya Wiki ya Mwanakatavi. Katika ziara hiyo, alipata maelezo kuhusu huduma na elimu inayotolewa kwa wakulima kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji.
Akizungumza baada ya kutembelea mabanda hayo, alisema ameelezwa kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima, zikiwemo kushuka kwa bei za mazao ya pamba, ufuta na mbaazi, pamoja na kuporomoka kwa bei ya tumbaku mwaka huu ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Alisema hali hiyo imekuwa na athari za kiuchumi kwa wakulima wa mazao hayo, lakini akasisitiza kuwa changamoto hizo hazipaswi kuwakatisha tamaa au kuwafanya waache shughuli za kilimo.
Badala yake, aliwataka kuendelea kulima huku wakizingatia elimu na kutumia mbinu bora za uzalishaji zitakazowawezesha kuongeza mavuno na kuzalisha mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Katavi, Faridu Abdalah, alisema kupitia maonesho ya Wiki ya Mwanakatavi wamefanikiwa kuwafikia wakulima wengi kwa kuwapatia elimu kuhusu mbinu bora za kilimo.
Alisema matarajio yao ni kuona elimu hiyo ikitumika kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuchangia kuimarisha sekta ya kilimo mkoani Katavi.
Leave a Reply