
Na Mwandishi Wetu
Watu wawili wamejisalimisha kwa hiari na kukabidhi silaha mbili pamoja na risasi 22 kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, katika siku ya mwisho ya kampeni ya usalimishaji wa silaha haramu iliyohitimishwa Oktoba 31, 2026.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, imeeleza kuwa silaha zilizokabidhiwa ni bunduki aina ya Long Rifle .22 iliyokuwa na risasi tatu na bastola aina ya Pistol Revolver .38 Webley iliyokuwa na risasi 19.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, silaha hizo zilikabidhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kudhibiti umiliki na matumizi ya silaha kinyume cha sheria pamoja na kuimarisha usalama katika jamii.
Kamanda Kuzaga amesema kampeni hiyo ililenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kumiliki silaha bila kufuata taratibu za kisheria, sambamba na kuwahamasisha wenye silaha hizo kuzisalimisha kwa hiari.
Amewataka wananchi ambao bado wanamiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha katika vituo vya polisi, ofisi za Serikali au kwa watendaji wa kata.
Aidha, ameonya kuwa baada ya kumalizika kwa kampeni hiyo, Jeshi la Polisi litafanya misako kubaini, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaobainika kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Kampeni ya usalimishaji wa silaha haramu ilizinduliwa rasmi Septemba Mosi, 2026, na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ikiwa na lengo la kupunguza umiliki wa silaha kinyume cha sheria na kuimarisha usalama nchini. Kampeni hiyo ilitarajiwa kuhitimishwa Oktoba 31, mwaka huu.
Leave a Reply