
Na Happy Milion
Wananchi jijini Mbeya wameipongeza Serikali kwa kuanza kuweka lami katika barabara kuu ya TANZAM, kuanzia eneo la Mbeya Pazuri hadi Mama John, wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kumaliza kero ya vumbi iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.
Uwekaji wa lami katika eneo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa barabara ya TANZAM kutoka njia mbili hadi nne, unaolenga kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji pamoja na kurahisisha shughuli za kiuchumi jijini Mbeya.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema kuwa hadi sasa jumla ya kilomita mbili zimekamilika kuwekwa lami, kuanzia Mbeya Pazuri hadi eneo la Mama John, huku kazi zikiendelea katika maeneo mengine.
Baadhi ya wananchi waliozungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema uwekaji wa lami utasaidia kupunguza vumbi ambalo limekuwa likiwaathiri wakazi wa maeneo hayo na watumiaji wa barabara hiyo.
Aidha, wananchi hao wameipongeza Serikali kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo, wakieleza kuwa utakapokamilika, utarahisisha usafiri na usafirishaji, kupunguza changamoto za usafiri na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi ndani ya Jiji la Mbeya.
Hatua hiyo inafuatia maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya, Oktoba 16 na 17, 2026, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi.
Leave a Reply