
Na Juma John Elisha
Kaka wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ambaye ni Wakili Allute Lissu Mughwai, amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 1, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Siriani jijini Arusha.
Akizungumzia kifo cha marehemu, dada yake, Rose Masesa, amesema Allute alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa kwa muda mrefu, ingawa hali yake ya kiafya ilikuwa imeanza kuimarika kabla ya kuzidiwa ghafla siku chache zilizopita.
Masesa amesema familia ilikuwa na matumaini ya kuona marehemu akiendelea kupata nafuu na hata kusafiri kwenda Dar es Salaam, lakini hali yake ilibadilika ghafla na kulazimika kukimbizwa hospitalini.
Amesema hali hiyo imeishtua familia kwa kuwa marehemu alikuwa akionyesha dalili za kuimarika kiafya.
“Ndiyo mambo ya vifo, vinakuja wakati wowote. Alizidiwa ghafla, akakimbizwa hospitali. Alikuwa anaumwa muda mrefu, lakini hii ya kuzidiwa imetushtua sana na alikuwa anaendelea vizuri na tulijua anakuja Dar. Tunamshukuru Mungu,” amesema Masesa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia, shughuli za msiba zinafanyika nyumbani kwa marehemu jijini Arusha. Hata hivyo, ratiba rasmi ya mazishi ilikuwa bado haijatolewa hadi wakati habari hii inaandaliwa.
Kifo cha Wakili Allute Lissu Mughwai ni pigo kwa familia yake, ndugu, jamaa na marafiki, huku akifahamika pia kutokana na uhusiano wake wa kifamilia na Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Leave a Reply