
Na Jastini Bukebuke, Geita
Wazazi na walezi wametakiwa kuepuka kuwaozesha au kuwapa ajira vijana wanaohitimu elimu ya kidato cha nne, badala yake wawape fursa ya kuendelea na masomo ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu na kujenga maisha bora ya baadaye.
Wito huo umetolewa jana na Mkaguzi wa Polisi, INSP Gabriel Rweikiza, wakati wa mahafali ya tatu ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Nyalwanzaja, iliyopo Kata ya Nyalwanzaja, Tarafa ya Busanda, Wilaya ya Geita, mkoani Geita.
Akizungumza katika mahafali hayo, INSP Rweikiza aliwataka wanafunzi kuzingatia maadili mema, kujitambua na kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na malengo chanya ili kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha na mustakabali wao.
Alisisitiza kuwa kuhitimu elimu ya kidato cha nne si mwisho wa safari ya elimu, bali ni hatua muhimu inayofungua milango ya fursa nyingine za kielimu na kimaisha. Hivyo, aliwahimiza wanafunzi kutokata tamaa katika safari ya kutimiza ndoto zao.
Aidha, aliwataka wazazi na walezi kuendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono vijana hao kwa kuwapatia fursa ya kujiendeleza kielimu, badala ya kuwahusisha na majukumu ya ndoa au ajira katika umri ambao bado wanahitaji kujenga msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyalwanzaja, Isack Msuka, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu kwa wanafunzi na wananchi, akieleza kuwa elimu hiyo ina mchango mkubwa katika kuwajengea vijana uelewa kuhusu maadili mema, uwajibikaji na namna ya kujilinda dhidi ya vitendo vinavyoweza kuathiri maisha yao.

Leave a Reply