
Na Jastini Bukebuke, Geita
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Geita, ACP Mathew Msuyale, amewapongeza madereva wa pikipiki na bajaji walioshiriki mafunzo ya udereva kwa hiari, yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu usalama barabarani wanapotumia vyombo hivyo vya moto, pamoja na kuwawezesha kupata leseni za udereva.
Pongezi hizo zimetolewa leo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo ya awamu ya kwanza kwa madereva wa pikipiki na bajaji, iliyofanyika katika Ukumbi wa Polisi wilayani Geita.
Katika hatua nyingine, ACP Msuyale amefungua rasmi mafunzo ya udereva kwa madereva wa magari makubwa na mabasi, huku akiwataka washiriki kuzingatia na kutumia ipasavyo maarifa watakayoyapata ili kuboresha usalama barabarani. Aidha, amewasisitiza madereva kuacha tabia ya kupuuza alama za barabarani na kuvunja sheria za usalama barabarani.

Kwa upande wake, Katibu wa Madereva wa Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Geita, Fredy Mngeta, amelishukuru Jeshi la Polisi pamoja na Chuo cha DVTC Ufundi Chato kwa kutambua umuhimu wa kutoa mafunzo kwa madereva na wadau wa usafirishaji.
Amesema ushirikiano huo wa kutoa elimu kwa gharama nafuu umekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha madereva kupata ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Leave a Reply