
Na Mariam Kondo
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amewataka wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuongeza kasi ya kazi ili kufidia muda uliopotea kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora, mazingira na masuala ya kijamii.
Balozi Omar alitoa wito huo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa reli hiyo katika vipande vya tatu, nne na tano. Alisema Serikali inataka kuona mradi huo ukitekelezwa kwa kasi zaidi ili kufikia malengo ya kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi kupitia mtandao wa reli ya kisasa.
Alisema licha ya changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo, ambazo zimeelezwa na mkandarasi, mshauri elekezi na Shirika la Reli Tanzania (TRC), Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la kuharakisha ujenzi.

Balozi Omar aliipongeza TRC, Wizara ya Fedha na wataalamu wengine kwa kubuni utaratibu mbadala uliosaidia kuondoa baadhi ya vikwazo na kuimarisha kasi ya utekelezaji wa mradi huo.
“Kwa mujibu wa taarifa, utekelezaji wa kipande cha tatu umefikia asilimia 16.1 na kipande cha nne asilimia 10.08. Haya ni maendeleo mazuri, ingawa juhudi zaidi zinahitajika kuongeza kasi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati,” alisema.
Alibainisha kuwa ujenzi wa reli hiyo una umuhimu mkubwa wa kimkakati katika kuunganisha maeneo ya mashariki na magharibi mwa Tanzania, kuanzia Dar es Salaam kupitia Dodoma hadi Mwanza na kuendelea Kigoma.

Alisema kukamilika kwa kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, pamoja na maendeleo ya ujenzi wa kipande cha tano kuelekea Mwanza, ni hatua muhimu. Hata hivyo, alisisitiza kuwa vipande vinavyounganisha maeneo hayo, ikiwemo kipande cha tatu, vina mchango mkubwa katika kukamilisha mtandao wa reli hiyo.
“Tusipokamilisha vipande vinavyounganisha maeneo haya, hatutakuwa tumefikia kikamilifu malengo makubwa ya mradi huu ya kuiunganisha nchi kutoka mashariki hadi magharibi,” alisema Balozi Omar.
Aidha, aliwataka wakandarasi wanaotekeleza sehemu mbalimbali za mradi huo kukamilisha kazi walizokabidhiwa kwa wakati, akisisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayatapimwa kwa upatikanaji wa fedha pekee, bali pia kwa kuzingatia muda wa utekelezaji na ubora wa kazi.
Katika hatua nyingine, Balozi Omar alisisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya mazingira na kijamii wakati wa utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa ni miongoni mwa masharti muhimu yanayosisitizwa na taasisi za kimataifa zinazofadhili miradi ya maendeleo kupitia mikopo.
Alisema Serikali na washirika wake wa maendeleo wanapaswa kuhakikisha masuala hayo yanashughulikiwa mapema ili kuzuia changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji au baada ya fedha za mradi kutolewa.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya Wizara ya Fedha, TRC, wakandarasi, washauri elekezi na wataalamu wengine ili kuhakikisha mradi wa SGR unakamilika kwa ufanisi na kutoa mchango uliokusudiwa katika kukuza uchumi, kurahisisha usafirishaji na kuimarisha maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema ziara hiyo ya pamoja na Waziri wa Fedha imelenga kuimarisha ushirikiano kati ya wizara hizo mbili katika kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo zinatumika ipasavyo.
Alisema ni muhimu kwa Wizara ya Fedha, inayosimamia upatikanaji wa fedha, kujionea maendeleo ya miradi inayofadhiliwa, huku Wizara ya Uchukuzi ikiendelea kusimamia utekelezaji wake.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Shiwa, alieleza mikakati ya shirika hilo katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi, ikiwemo kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza.
Wakati huohuo, Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Salim Omary Salim, alisema utekelezaji wake unazingatia masharti ya mkataba, viwango vya ubora na matakwa ya kimazingira ili kuhakikisha unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.
Leave a Reply