
Na Ummy Kondo, Dodoma
Wanafunzi wapya na wanaoendelea wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wametakiwa kuwajibika katika masomo na kuwa na nidhamu ili wasome na kuhitimu kwa wakati.
Wito huo ulitolewa na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Alex Makulio katika hotuba yake ya ukaribisho kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea kwa Mwaka wa masomo wa 2025/2026.
Alisema wanapaswa kuwa makini na masomo yao kila wakati na kufuatilia programu zinazoendelea za ufundishaji, hususani mihadhara ya inayofundishwa kwa njia ya mtanadao kupitia programu tumizi ya Zoom.
“Napenda kuwakumbusha kwamba kusoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kunahitaji nidhamu binafsi na kujituma”, alisema Profesa Makulilo.
Aidha alisema chuo kitakuwa kinatoa ratiba ya ufundishaji mara kwa mara ili wanafaunzi wafuatilie hivyo kutoachwa katika masomo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Mkoa cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dodoma, Dr.Mohamed Msoroka alisema kusoma kwa mafanikio kunawezekana kwa kila mtu lakini zaidi ni kwa wale wanaojituma huku akisisitiza watumie muda wao vizuri.
“Jihusishe kikamilifu katika vipindi na mihadhara ya mtandaoni na vile vya ana kwa ana na usisite kutafuta msaada unapouhitaji kwa kuwa milango yetu iko wazi wakati wote”, alisema Dkt.Msoroka.

Alisema kwa kuwa wadahiliwa wengi ni watu wazima, wenye familia, ajira, na majukumu mengine ndiyo maana Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilianzishwa ili kuwapatia urahisi, uhuru, na fursa ya kuendelea na elimu ya juu bila kuathiri majukumu yao.
“Mafanikio katika ujifunzaji kwa njia ya elimu huria na ya masafa yanahitaji nidhamu binafsi, kujitolea, na uwezo mzuri wa kusimamia muda”, alisema Dkt. Msoroka.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Kituo cha Mkoa cha Dodoma, Sabina Mpigauzi anayesomea ualimu alisema aliamua kuhudhuria mafunzo elekezi ili kupata taarifa za ziada kuhusu masomo ili kwenye sehemu ambazo hana ufahamu nazo ili kuendelea vyema na masomo yake.
Aidha, alitoa wito kwa watumishi wa umma na sekta binafsi kujiendeleza kitaaluma kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwani kinawawezesha kuendelea na masomo bila kuathiri majukumu yao mengine kama ajira. malezi na uangalizi wa familia zao.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni chuo kikuu cha umma kinachotoa elimu kupitia mfumo wa masafa na huria kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa kwake na kwamba kinatoa huduma hiyo ndani na nje ya nchi.


Leave a reply to heroic88a7c6bbb0 Cancel reply