Na Cosmas Msuha
WOMESA imewataka wanawake kutumia fursa mbalimbali za ajira zinazopatikana katika sekta ya bahari, ambazo zinagusa nyanja tofauti za kijamii na kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wa TASAC, Mwatano Maganga, wakati wa kongamano la maadhimisho ya umoja huo lililofanyika Bagamoyo, mkoani Pwani.
Maganga alisema sekta ya bahari ni miongoni mwa sekta zinazotoa fursa nyingi za kiuchumi duniani kutokana na uwepo wa mnyororo mpana wa thamani unaowezesha shughuli mbalimbali za uchumi kufanyika kutoka eneo moja hadi jingine.
Aidha, mdau wa sekta ya bahari, Dkt. Judith Mhina, aliwataka wanawake nchini na barani Afrika kujikita katika ajira zinazotokana na sekta hiyo ili kuchangia ukuaji wa uchumi binafsi na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WOMESA, Fatma Masenene, alisema maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kutoa nafasi ya wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya bahari kukutana, kubadilishana uzoefu, na kuelimishana kuhusu fursa zilizopo.
Aliongeza kuwa mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo washiriki walitembelea Chuo cha Uvuvi cha Mbegani pamoja na shule za sekondari za Asanari Damji, Zinga, Makurunge Coast na Kongo kwa ajili ya kuwaelimisha wanafunzi kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya bahari.
Washiriki wa kongamano hilo kutoka taasisi mbalimbali walishauri mamlaka zinazohusika na usimamizi wa sekta ya bahari nchini kuongeza juhudi katika utoaji wa fursa za ajira kwa wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya sekta hiyo.
Leave a comment