
Na George Mwamba
Viongozi na maafisa kutoka taasisi mbalimbali za usalama za Tanzania na Msumbiji wamekutana mjini Songea kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu makosa na uhalifu wa kuvuka mipaka, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya kiusalama.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza jana katika Ukumbi wa Heritage Cottage, Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, umezikutanisha pande hizo mbili kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti uhalifu wa kuvuka mipaka na kuimarisha usalama wa wananchi.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Perres Magiri, alisema ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Msumbiji ni muhimu katika kudumisha amani, usalama na utulivu katika maeneo ya mipakani.
Alisema mikutano ya aina hiyo imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga mahusiano mazuri, kuimarisha mawasiliano na kutafuta suluhisho la pamoja kwa changamoto za kiusalama zinazojitokeza katika maeneo ya mipaka.
Kwa mujibu wa Magiri, washiriki wa mkutano huo wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usalama wa wananchi, udhibiti wa uhalifu wa kuvuka mipaka, usimamizi wa mipaka na namna ya kuendeleza ushirikiano wa kiutendaji kati ya vyombo vya usalama vya Tanzania na Msumbiji kwa manufaa ya mataifa yote mawili.
Kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco Chilya, alimtambulisha Kamanda wa Jimbo la Niassa, Kamishna Msaidizi wa Polisi Celestino Albano Vianeque, kwa washiriki wa mkutano.


Leave a comment