Na Cosmas Msuha

Wananchi wa Kimara, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, wanatarajia kuondokana na changamoto za usafiri baada ya ujenzi wa Barabara ya TRA–King’ong’o unaoendelea kwa kiwango cha zege kufikia hatua nzuri.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Catherine Sungura, wakati wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.

Alisema katika ujenzi wa barabara hiyo zimebaki kilomita 1.6, ambapo mita 800 zinatarajiwa kujengwa kuanzia Julai mwaka huu, huku sehemu iliyosalia ikikamilishwa katika awamu inayofuata.

Sungura alisema TARURA itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri, kuimarisha mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumzia huduma zinazotolewa katika banda la TARURA, alisema wananchi wanaowasilisha kero zao huunganishwa moja kwa moja na mameneja wa mikoa au wilaya husika ili kupata majibu na ufumbuzi kwa wakati.

Kwa upande wake, mkazi wa Kimara, Sarah James Joseph, alisema ameridhishwa na maelezo aliyopata kuhusu maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo baada ya kuwasiliana na Meneja wa TARURA Wilaya ya Ubungo kupitia banda la wakala huo.

Tangu kuanza kwa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, zaidi ya wananchi 300 wametembelea banda la TARURA kupata taarifa na ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara nchini.

Posted in

Leave a comment