Na Cosmas Msuha

Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na kampuni mbili kutoka Japan ili kufungua fursa za soko la biashara ya kaboni kupitia Mpango wa Uratibu wa Pamoja wa Mikopo (JCM).

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo iliyofanyika Juni 25, 2026, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Mayungi, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kupitia uwekezaji katika nishati safi, biashara ya kaboni na usimamizi endelevu wa taka.

Dkt. Mayungi alisema ushirikiano huo pia unalenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya mazingira na maendeleo endelevu, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kijani.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Biashara ya Kaboni (NCMC), Ngenda Kigaraba, alisema mfumo wa utoaji wa mikopo ya pamoja utachangia kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kukuza biashara ya kaboni na kuongeza mapato ya Serikali kupitia uwekezaji wa miradi rafiki kwa mazingira.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya 3T kutoka Japan, Kan Shimizu, alisema Tanzania itanufaika kwa kiwango kikubwa kupitia ushirikiano huo, hususan katika kuendeleza miradi ya utunzaji wa mazingira na biashara ya kaboni, ambayo pia itasaidia kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Makubaliano hayo kati ya NCMC na kampuni hizo za Japan yanatarajiwa kuchochea ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya mazingira, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, hususan nguzo ya tatu inayosisitiza ukuaji wa uchumi unaozingatia maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira.

Posted in

Leave a comment