Na Jastini Bukebuke

Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Geita (TPF-NET) umetembelea na kutoa msaada katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Bin Ghanimu kilichopo Bwanga, Wilaya ya Chato, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuwafariji na kusaidia watoto wenye uhitaji katika jamii.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Bwanga, ASP Neema Nhaluke, alisema TPF-NET imeendelea kuwa daraja la ulinzi, upendo na matumaini kwa jamii, hususan kwa watoto wenye mazingira magumu. Alisisitiza kuwa jukumu la askari wanawake haliishii katika kulinda usalama pekee, bali linajumuisha pia kushiriki katika shughuli za kijamii zinazogusa makundi yenye uhitaji.

ASP Nhaluke aliwataka walezi kuendelea kusimamia maadili, uzalendo na malezi bora ili kuwajengea watoto msingi imara wa kuwa raia wema na wenye manufaa kwa taifa.

Kwa upande wao, Wakaguzi wa Polisi Paschazia Nunda na Shida Samweli waliwahimiza watoto hao kuzingatia nidhamu na maadili mema, wakieleza kuwa tabia njema ndiyo msingi wa kufikia ndoto na malengo yao ya maisha.

Aidha, walitoa wito kwa watoto na walezi kutovumilia vitendo vya unyanyasaji na ukatili, wakisisitiza umuhimu wa kuripoti matukio hayo kwa mamlaka husika bila hofu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Naye Mkuu wa Shule na Mlezi wa kituo hicho, Seleiman Shila, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa upendo, faraja na msaada walioutoa, akiahidi kuendelea kuwalea watoto hao katika misingi ya nidhamu, maadili na elimu ili wawe tegemeo la taifa siku zijazo.

Posted in

Leave a comment