
Na Yusra Temba
Harakati za kukuza utalii nchini zimeendelea kushika kasi baada ya mamia ya washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania kushiriki mbio za Arusha Tourism Marathon zilizofanyika jana ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha, zikilenga kuhamasisha utalii kupitia michezo.

Mashindano hayo yalijumuisha mbio za kilometa 2.5, 5, 10 na 21, mbio za baiskeli, burudani ya muziki, michezo ya watoto pamoja na shughuli mbalimbali zilizowapa washiriki fursa ya kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Witness Shoo, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema mbio hizo zimekuwa jukwaa muhimu la kutangaza utalii kwa kuwaunganisha wananchi na wageni na vivutio vya asili vinavyopatikana nchini.
Alisema matukio yanayounganisha michezo na utalii yana mchango mkubwa katika kuitangaza Tanzania kimataifa na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine ya vivutio vya utalii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Ruaha Tourism Marathon, Cornell Magoti, alisema lengo la mbio hizo ni kuunganisha sekta ya michezo na utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya Tanzania na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii.
Baadhi ya washiriki wa mbio hizo walieleza kufurahishwa na mandhari ya kuvutia pamoja na vivutio mbalimbali walivyopata fursa ya kuviona ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha, wakisema tukio hilo limewapa uzoefu wa kipekee na kuwahamasisha kuendelea kutembelea maeneo ya utalii nchini.
Waandaaji wa mbio hizo walieleza kuwa wanaendelea kutumia michezo kama jukwaa la kuitangaza Tanzania, wakiamini kuwa matukio ya aina hiyo yanaongeza mwamko wa utalii wa ndani na kuvutia wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Leave a comment