Na Jastini Bukebuke, Geita

Mafundi ujenzi wapatao 460 kutoka mikoa ya Geita na Mwanza wamehimizwa kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu ili kujenga imani kwa wateja, kuboresha huduma wanazotoa na kuinua ustawi wa maisha yao.

Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, wakati akifungua semina maalum iliyoandaliwa na Kampuni ya Magic Builders International ya Dar es Salaam. Semina hiyo ilifanyika jana katika Ukumbi wa Golden Social Hall uliopo Manispaa ya Geita.

Akizungumza katika semina hiyo, SACP Jongo aliwakumbusha mafundi hao umuhimu wa kuzingatia sheria katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku, kuepuka vitendo vya uhalifu na ulaghai dhidi ya wananchi, pamoja na kutoshirikiana na wahalifu katika wizi wa vifaa vya ujenzi.

Alisisitiza kuwa mafundi wanapaswa kutekeleza majukumu yao katika mazingira salama yanayozingatia sheria, huku wakidumisha amani, utulivu na mahusiano mema na jamii ili kuchochea maendeleo ya sekta ya ujenzi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Magic Builders International, David Barongo, aliwahimiza mafundi hao kuendelea kujiendeleza kitaaluma kwa kupata mafunzo kutoka katika vyuo vinavyotambulika na mamlaka husika ili kuongeza maarifa, ujuzi na uzoefu unaowawezesha kutoa huduma bora na zenye ushindani.

Barongo pia alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kushiriki semina hiyo na kutoa elimu iliyolenga kuimarisha uzingatiaji wa sheria, maadili ya kazi na usalama katika sekta ya ujenzi.

Alisema ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi una mchango mkubwa katika kuwajengea mafundi uwezo, kuongeza taaluma na kukuza sekta ya ujenzi nchini.

Posted in

Leave a comment