
Na Farida Mkumba
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amepongeza mchango wa Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) katika kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kusimamia na kuendeleza utawala wa Serikali za Mitaa nchini.
Magoti alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la LGTI katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Alisema LGTI imeendelea kujijengea sifa kwa kutoa elimu na mafunzo yenye ubora, yaliyowezesha kuzalishwa kwa wataalamu wenye weledi wanaochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Serikali za Mitaa na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Magoti alisema anajivunia kuwa mmoja wa wahitimu wa chuo hicho, akibainisha kuwa elimu aliyoipata imekuwa msingi muhimu katika safari yake ya utumishi wa umma.
“Elimu niliyopata LGTI imekuwa msingi imara wa utendaji wangu wa kazi na ndiyo imenisaidia kufikia mafanikio haya niliyoyapata katika utumishi wa umma,” alisema Magoti.
Aidha, aliwataka vijana na watumishi wa umma kuendelea kuthamini elimu na mafunzo ya kitaaluma, akisisitiza kuwa taasisi kama LGTI zina nafasi kubwa katika kujenga watumishi wenye ujuzi, maadili na uwezo wa kusimamia maendeleo ya nchi.
Akihitimisha ziara yake katika banda la chuo hicho, Magoti alikabidhiwa zawadi maalum yenye nembo ya LGTI kama kumbukumbu ya kutembelea banda hilo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Maonesho ya SABASABA yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha huduma, bidhaa na mafanikio yao. Kupitia maonesho hayo, LGTI inaendelea kutumia fursa hiyo kutangaza programu zake za mafunzo na kuonesha mchango wake katika kuimarisha utawala wa Serikali za Mitaa nchini.
Leave a comment