
Na Yusra Temba
Mzize Foundation kwa kushirikiana na GSM Foundation imeandaa Tamasha la ‘Washike Mkono’, lililofanyika jana katika Uwanja wa Samora mkoani Iringa, likiwa na lengo la kukusanya rasilimali kwa ajili ya kuwapatia madereva wa bodaboda kofia ngumu (helmeti) na kuchangia vifaa tiba katika vituo mbalimbali vya afya mkoani humo.
Mgeni rasmi katika tamasha hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ambaye aliungana na mamia ya wakazi wa mkoa huo kushiriki tukio hilo lililolenga kuhamasisha mshikamano wa jamii kupitia michezo na shughuli za kijamii.
Mbali na kampeni ya kuchangisha rasilimali, Mzize Foundation ilitoa mafuta bure kwa madereva wa bodaboda walioshiriki tamasha hilo ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wao katika jamii na kuhamasisha usalama barabarani.
Akizungumza baada ya tamasha hilo, mshambuliaji wa Klabu ya Young Africans (Yanga SC) na Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Clement Mzize, aliwashukuru wakazi wa Mkoa wa Iringa kwa mwitikio mkubwa waliouonesha na kueleza kufurahishwa na mafanikio ya tukio hilo.
“Kwa kweli nina furaha sana. Matarajio niliyokuwa nayo yametimia kwa kiwango kikubwa. Watu wamejitokeza kwa wingi kunipa ushirikiano kwa sababu ni ndugu yao. Huu ni mwanzo mzuri, na naamini mambo mengi mazuri zaidi yanakuja,” alisema Mzize.
Kwa upande wake, Msemaji wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, aliwapongeza wakazi wa Mkoa wa Iringa kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki tamasha hilo, akisema mwitikio huo unaonesha mshikamano mkubwa wa wananchi katika kuunga mkono shughuli zenye manufaa kwa jamii.
Tamasha hilo lilianza kwa mazoezi ya pamoja yaliyowakutanisha wananchi na wadau mbalimbali, kisha kufuatiwa na mchezo wa utangulizi kati ya Iringa All Stars Veterans na Ruaha National Park, uliomalizika kwa sare ya mabao 1-1.
Baadaye kulichezwa mechi ya hisani kati ya Timu ya Mzize na Timu ya Oscar, ambapo Timu ya Mzize iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Tamasha hilo lilifanikishwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo Ruaha National Park, K4S Security, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, ASAS pamoja na taasisi nyingine zilizojitokeza kuunga mkono jitihada za Mzize Foundation za kutumia michezo kama chachu ya maendeleo na ustawi wa jamii.


Leave a comment