Na George Gabriel

Timu ya Nanyumbu Veterans imezindua rasmi jezi zake mpya katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Lindi Veterans uliochezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mangaka, Wilaya ya Nanyumbu.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya mabao 1-1, huku ukishuhudiwa na mashabiki wengi na kuambatana na ushindani mkubwa. Lengo la mchezo huo lilikuwa kuimarisha afya, umoja na mshikamano miongoni mwa wanamichezo na jamii.

Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi huo alikuwa Diwani wa Kata ya Mangaka, Salvatory Lyimo, ambaye aliipongeza Nanyumbu Veterans kwa hatua ya kuzindua jezi mpya na kuendelea kushiriki shughuli za michezo zinazochochea afya, urafiki na ushirikiano wa wananchi.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Nahodha wa Nanyumbu Veterans, Hassan Simoje, alimshukuru Diwani Lyimo kwa ushirikiano na uungaji mkono wake, akisema umeongeza ari kwa wachezaji na kuhamasisha maendeleo ya michezo katika kata hiyo.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Diwani kwa kuwa nasi wakati wote. Mchango wake umetupa nguvu na motisha wa kuendelea kuitangaza Mangaka kupitia michezo,” alisema Simoje.

Kwa upande wake, shabiki wa timu hiyo, Matajabu Juma, alisema uzinduzi wa jezi mpya ni hatua muhimu kwa Nanyumbu Veterans na utaongeza hamasa kwa wachezaji pamoja na mashabiki.

“Tunajivunia kuona timu yetu inaendelea kupiga hatua. Tunampongeza Diwani kwa kuendelea kuwa karibu na timu, na tunaamini ushirikiano huu utaifanya Nanyumbu Veterans kufikia mafanikio makubwa zaidi,” alisema Juma.

Mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo walieleza kufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu zote mbili, wakiahidi kuendelea kuiunga mkono Nanyumbu Veterans katika michezo ijayo. Walisisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha afya, urafiki na maendeleo ya jamii.

Posted in

Leave a comment