Na Mwandishi Wetu

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kwa kushirikiana na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), wamezindua programu maalum ya kuwajengea uwezo na kuwathibitisha Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Alex Makulilo, alisema programu hiyo si semina ya kawaida, bali ni mafunzo ya kina yatakayojumuisha nadharia na vitendo.

Alisema uteuzi wa Afisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi pekee hautoshi kumwezesha kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

“Msingi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kukichagua Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni uwezo wake wa kutoa mafunzo hayo bila kuathiri utekelezaji wa majukumu ya washiriki ya kila siku,” alisema Prof. Makulilo.

Prof. Makulilo alisema awamu ya kwanza ya programu hiyo itaanza rasmi tarehe 10 Agosti 2026. Mafunzo hayo yatakuwa na moduli tano, yataendeshwa kwa muda wa siku 14, na kila mshiriki atachangia Sh milioni 2.5.

Aliongeza kuwa baada ya mafunzo, washiriki watafanyiwa tathmini ya kina kabla ya kuthibitishwa rasmi na PDPC.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, alisema licha ya taasisi nyingi kutekeleza matakwa ya sheria kwa kuteua Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi, imebainika kuwa maafisa hao wana viwango tofauti vya taaluma na uelewa kuhusu dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi.

Alisema ushirikiano kati ya PDPC na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni msingi imara wa kujenga wataalamu wenye weledi katika fani ya ulinzi wa taarifa binafsi.

“Mafunzo haya yapo kwa mujibu wa sheria na ni lazima kwa kila Afisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi aliyeteuliwa kuyapata ili kuhakikisha anatekeleza kikamilifu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi,” alisema Dkt. Mkilia.

Dkt. Mkilia aliwataka viongozi wa taasisi zote kuwawezesha Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa taasisi zao kushiriki katika programu hiyo ili kuimarisha utawala bora na kujenga imani ya wananchi katika huduma zinazotolewa.

Alisema dhamira ya Tume ni kuona Tanzania inakuwa na Maafisa Ulinzi wa Taarifa Binafsi wenye ujuzi, weledi na umahiri wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, huku wakilinda faragha na taarifa za wananchi.

Posted in

Leave a comment