Na George Gabriel

Wananchi wa Kijiji cha Masugulu, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, wameiomba Serikali kuhakikisha Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma–Mangaka unakamilika kwa wakati ili waanze kunufaika na huduma ya maji safi na salama.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwanahawa Juma alisema licha ya mradi huo kuanza kutekelezwa, bado wanaiomba Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji ili kutimiza ahadi ya kuwapatia maji ya uhakika na kuondoa kero ya muda mrefu.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuleta mradi huu mkubwa, lakini tunaomba ukamilike haraka kwa sababu tumekuwa tukiusubiri kwa muda mrefu tangu Rais alipotuahidi,” alisema Mwanahawa.

Naye Mzee Shaibu Lipindi alisema upatikanaji wa maji ya uhakika utapunguza adha ambayo wananchi wamekuwa wakikabiliana nayo kwa miaka mingi. Aliipongeza Serikali kwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.

Kwa upande wake, mwakilishi wa mkandarasi, AFCONS Infrastructure Ltd, alisema kampuni hiyo imepokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo. Aliahidi kuwa watafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, alimtaka mkandarasi kuongeza nguvu kazi, vifaa na rasilimali nyingine muhimu ili kuhakikisha mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 38.1 unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu na maeneo ya jirani.

Serikali imeendelea kusisitiza kuwa upatikanaji wa maji safi na salama ni miongoni mwa vipaumbele vyake katika kuboresha maisha na kuchochea maendeleo ya wananchi.

Maoni ya wananchi pamoja na agizo la Mkuu wa Mkoa kwa mkandarasi yalitolewa wakati wa ziara ya Kanali Donald Msengi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

Posted in

Leave a comment