Na Jastini Bukebuke

Walimu wa Shule ya Msingi Simbaguji, iliyopo Kata ya Kanyala, Wilaya ya Geita, wametakiwa kuimarisha usimamizi wa vilabu vya kupinga ukatili wa kijinsia shuleni ili viendelee kuwajengea wanafunzi uelewa wa haki zao, ujasiri wa kutoa taarifa, maadili mema na uwezo wa kujilinda dhidi ya ukatili pamoja na vitendo vingine vinavyohatarisha usalama wao.

Wito huo ulitolewa jana na Polisi Kata wa Kanyala, Inspekta Said Juma, alipokuwa akitoa elimu ya kinga kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumza katika elimu hiyo, Inspekta Juma alisema vilabu vya kupinga ukatili wa kijinsia ni nyenzo muhimu katika kuwafundisha wanafunzi kutambua haki zao, kutoa taarifa kwa wakati wanapobaini viashiria vya ukatili na kujiepusha na mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama wao.

Aidha, aliwataka walimu kuhakikisha vilabu hivyo vinaendelea kufanya kazi kwa ufanisi kupitia mikutano ya mara kwa mara, utoaji wa elimu endelevu na ushirikiano wa karibu kati ya shule, wazazi na jamii ili kuimarisha ulinzi wa watoto.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Simbaguji, Renatus Misago Chigunga, alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa elimu ya kinga shuleni.

Alisema ushirikiano huo unachangia kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu masuala ya usalama, kuimarisha maadili mema na kujenga mazingira salama na rafiki ya kujifunzia.

Posted in

Leave a comment