
Na Cosmas Msuha
Zaidi ya shilingi bilioni 38 zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku Serikali ikiahidi kuendelea kuboresha huduma za elimu, afya, maji, mawasiliano na miundombinu.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Laikala baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Vituo vya Afya vya Laikala na Sagara.
Akizungumza na wananchi wa kata za Laikala na Sagara, Waziri Kairuki alisema fedha hizo zimewezesha utekelezaji wa miradi katika sekta za afya, elimu, maji, kilimo, umwagiliaji na miundombinu.
“Hadi Juni 2026, Serikali imeelekeza shilingi bilioni 38.6 kutekeleza miradi ya afya, elimu, kilimo, umwagiliaji na miundombinu mingine ya maendeleo katika Wilaya ya Kongwa,” alisema Kairuki.
Aliongeza kuwa Serikali imejenga zaidi ya madarasa 640, maabara za sayansi karibu 50 na kuajiri walimu wa kutosha ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Aidha, aliahidi kupeleka kompyuta 44 katika shule mbili za wilaya hiyo pamoja na kuendelea kujenga madarasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa teknolojia.
Katika sekta ya maji, alisema upatikanaji wa huduma hiyo wilayani Kongwa umefikia asilimia 76.8, huku Serikali ikijiandaa kuchimba visima 19 katika vijiji ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya maji safi na salama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Saimon Mayeka, alisema wilaya hiyo imepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za jamii. Alieleza kuwa idadi ya shule za sekondari imeongezeka kutoka 26 hadi 41 baada ya kujengwa shule mpya 15, huku ongezeko la vituo vya afya likichangia kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na watoto.
Kwa mujibu wa Mayeka Wilaya ya Kongwa ina jumla ya shule za sekondari 45, zikiwemo 39 za Serikali na sita za binafsi.
Leave a comment