Na Jastini Bukebuke

Mkuu wa Kituo cha Polisi Kasamwa, Inspekta Said Juma, akishirikiana na askari wa kituo hicho, wamewafariji wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Kasamwa kwa kuwapa pole na kuwakabidhi mahitaji muhimu.

Tukio hilo lilifanyika Julai 25, 2026, katika Kituo cha Afya Kasamwa, Wilaya ya Geita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi kuendelea kuwa karibu na wananchi na kuimarisha mahusiano mema kupitia falsafa ya Polisi Jamii.

Akipokea msaada huo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kasamwa, Dkt. Emmanuel Ziragira, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuonesha moyo wa kujali na kuwafariji wagonjwa. Alisema matendo hayo yanawapa faraja na kuongeza matumaini kwa wananchi wanaopitia changamoto za kiafya.

Kupitia tukio hilo, Jeshi la Polisi limeendelea kudhihirisha kuwa jukumu lake halijikiti katika kulinda amani na usalama pekee, bali pia kujenga mahusiano ya karibu na jamii kupitia matendo ya huruma na huduma kwa wananchi.

Aidha, wananchi wamehimizwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa wakati, ili kuimarisha amani, usalama na utulivu katika jamii.

Posted in

Leave a comment