Na Damasi Kalembwe

Mashindano ya michezo ya Polisi Jamii Cup katika Mkoa wa Kinondoni yamezinduliwa rasmi Julai 27, 2026, katika viwanja vya michezo vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mgeni Rasmi, Mkuu wa Ushirikishwaji wa Jamii Mkoa wa Kinondoni, ACP Ally Wendo, aliyeambatana na Wakuu wa Himaya za Kinondoni na Kawe pamoja na Maafisa Watendaji wa Wilaya (DCEO) wa maeneo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya askari na washiriki wote, Koplo Itumbi Wambura alisema mashindano hayo ni fursa muhimu ya kuwakutanisha askari polisi na wananchi wanaowahudumia, hivyo kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Alisema lengo kuu la mashindano hayo ni kupata wachezaji mahiri watakaounda timu imara ya mkoa, sambamba na kuhamasisha afya bora kupitia mazoezi na michezo.

Aidha, mashindano hayo yanalenga kuongeza mshikamano, kufahamiana na kujenga ushirikiano wa dhati kati ya Jeshi la Polisi, jamii na wajumbe kutoka wilaya zote tano zinazoshiriki.

Katika siku ya ufunguzi, timu mbalimbali zilishiriki katika michezo ya riadha, kuvuta kamba, mpira wa miguu na mpira wa pete. Washiriki walionyesha ushindani mkubwa katika kila mchezo wakilenga kuzipatia ushindi himaya zao.

Matokeo ya michezo ya ufunguzi yalionesha Mkoa wa Kinondoni ukiibuka bingwa katika riadha na mpira wa pete. Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba, Himaya ya Kawe iliibuka mshindi, huku mchezo wa mpira wa miguu kati ya Kinondoni na Kawe ukimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Posted in

Leave a comment