
Na George Gabriel
Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu kupitia Kitengo cha Sheria imeendelea kutekeleza mpango wa kuwajengea uwezo wajumbe wa Mabaraza ya Kata kwa kutoa mafunzo ya uendeshaji wa mabaraza katika kata za Mikang’aula, Kamundi, Nangomba, Chipuputa, Masuguru, Nanyumbu na Mkonona.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Byera Nilo, alisema Mabaraza ya Kata ni nguzo muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kupitia usuluhishi wa migogoro mbalimbali katika jamii.
Alieleza kuwa migogoro ya ndoa inaweza kusuluhishwa katika Baraza la Kata kwa lengo la kufikia maridhiano kati ya pande husika na alisisitiza kuwa mamlaka ya kutoa talaka au kugawa mali za wanandoa yako chini ya vyombo vinavyotambuliwa kisheria.
Kwa upande wake, Afisa Sheria, Dora Kapinga, alisema katika migogoro ya ardhi, Baraza la Kata hutoa usuluhishi wa awali, na pale usuluhishi unaposhindikana, shauri hupelekwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kwa hatua zaidi za kisheria.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki baada ya mafunzo hayo, mmoja wa wajumbe wa Baraza la Kata, Fatuma Hussain, aliishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu pamoja na Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo yaliyowaongezea uwezo, maarifa na uelewa wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Alisema elimu waliyoipata itawasaidia kushughulikia migogoro kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, jambo litakalochangia kupunguza migogoro isiyo ya lazima na kuimarisha amani, umoja na haki katika jamii.
Mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa wajumbe wa Mabaraza ya Kata katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, ili kuboresha utoaji wa haki na usuluhishi wa migogoro katika jamii.
Washiriki walipatiwa elimu kuhusu majukumu ya Mabaraza ya Kata, taratibu za kupokea na kusikiliza mashauri, uandishi wa kumbukumbu na maamuzi ya mabaraza, pamoja na mipaka ya mamlaka yao kwa mujibu wa sheria.
Aidha, walipata mafunzo kuhusu usuluhishi wa migogoro ya ndoa na ardhi, huku wakisisitizwa kutenda haki kwa uadilifu, weledi na kuzingatia misingi ya sheria katika utekelezaji wa majukumu yao.

Leave a comment