Na Juma John Elisha

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuwa shauri la madai namba 14864, linalohusu mgawanyo wa mali za chama pamoja na maombi ya zuio dhidi yake, litatajwa kesho Jumatano, Agosti 5, 2026, saa 5:00 asubuhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, mbele ya Jaji Awamu Mbagwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, shauri hilo lililofunguliwa na Saidi Issa Mohammed na Ahmed Rashid Khamis linafikia hatua ya kutajwa baada ya kukamilika kwa majibizano ya kisheria kwa njia ya maandishi kati ya pande zote zinazohusika.

Katika taarifa hiyo, CHADEMA imewahimiza wanachama wake, wafuasi, wadau wa demokrasia pamoja na waandishi wa habari kujitokeza mahakamani kufuatilia mwenendo wa shauri hilo, ikisisitiza umuhimu wa umma kushuhudia hatua za mchakato wa kesi hiyo.

Kwa mujibu wa taratibu za mahakama, kutajwa kwa shauri ni hatua ya awali ya mchakato wa kesi ambapo mahakama hutoa maelekezo kuhusu hatua zinazofuata, ikiwemo ratiba ya usikilizwaji au masuala mengine ya kiutaratibu. Hivyo, kesho mahakama inatarajiwa kutoa maelekezo yatakayofuata kuhusu mwenendo wa shauri hilo.

Posted in

Leave a comment