
Na Pilastus Nyaulingo
Wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wameitaka Serikali kutambua kisheria mitandao ya jamii ya mawasiliano kama watoa huduma za kidijitali zisizo za kibiashara, wakisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuongeza upatikanaji wa intaneti katika maeneo ya vijijini na yaliyo pembezoni.
Wito huo umetolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na wadau wa TEHAMA, wawakilishi wa Serikali na mashirika ya kiraia katika kikao kilichojadili namna ya kupanua upatikanaji wa huduma za intaneti kwa jamii ambazo bado hazijahudumiwa ipasavyo.
Kikao hicho kiliandaliwa kwa ushirikiano wa Paradigm Initiative na Tanzania School of Community Networks, huku mjadala ukijikita katika umuhimu wa kuweka mazingira ya kisera na kisheria yatakayowezesha jamii kuanzisha na kuendesha mitandao yao ya mawasiliano.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk. Jabhera Matogoro, alisema mitandao hiyo inapaswa kutambuliwa chini ya Sera ya Taifa ya TEHAMA kama miundombinu ya kidijitali inayomilikiwa na jamii na isiyo ya kibiashara, pale inapokuwa imepewa leseni.
Kwa mujibu wa Dk. Matogoro, utambuzi huo ungezipa jamii unyumbufu zaidi wa kifedha katika kuendesha mitandao hiyo, badala ya kusimamiwa kwa mfumo unaotumika kwa kampuni za kibiashara za mawasiliano.
Alisema pia kuna umuhimu wa wananchi kuwa na ujuzi wa kidijitali ili uwekezaji katika miundombinu ya mtandao uweze kuleta matokeo chanya ya kiuchumi na kijamii.
“Ikiwa Tanzania inalenga kutimiza matarajio ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ni muhimu kuwawezesha wananchi kupata ujuzi wa kidijitali,” alisema Dk. Matogoro.
Alieleza kuwa mitandao ya jamii ya mawasiliano inaweza kusaidia kuwafikishia wananchi huduma za intaneti, huku uelewa wa matumizi ya teknolojia ukiwa muhimu katika kuhakikisha huduma hizo zinachangia maendeleo halisi ya kijamii na kiuchumi.
Afisa Mwandamizi wa Paradigm Initiative, Ihueze Nwobilor, alisema wanataka mitandao ya jamii itambulike katika sera na sheria za Tanzania kama huduma za jamii zisizo za kibiashara.
Alisema bila utambuzi huo, baadhi ya vijiji vinaweza kuendelea kubaki nje ya mchakato wa mabadiliko ya kidijitali nchini, licha ya kuwepo kwa teknolojia inayoweza kuwafikishia huduma za intaneti.
Kwa upande wake, Rose Ngunangwa, mmoja wa washiriki wa kikao hicho, alisema majadiliano hayo yamepanua uelewa wa washiriki kuhusu nafasi muhimu ambayo jamii zinaweza kuwa nayo katika kupunguza pengo la kidijitali kati ya watu wa mijini na vijijini.

Kwa mujibu wa Ngunangwa, hapo awali watu wengi waliamini kuwa jukumu la kupanua upatikanaji wa mtandao lilikuwa la kampuni za mawasiliano pekee, lakini kikao hicho kimeonesha kuwa jamii zenyewe zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho.
“Mitandao ya jamii imeonesha kwamba jamii zina uwezo wa kujijengea suluhisho zao. Tunachohitaji sasa ni mazingira wezeshi ya kisheria yatakayoruhusu ubunifu huu kuwafikia Watanzania wengi zaidi,” alisema Ngunangwa.
Wadau hao wanaamini kuwa utambuzi wa kisheria wa mitandao ya jamii ya mawasiliano utasaidia jamii kuwa na nafasi kubwa zaidi katika kujenga na kuendesha miundombinu ya mawasiliano kulingana na mahitaji yao.
Mitandao hiyo inaweza kuwa muhimu kwa wananchi wa maeneo ambayo hayajafikiwa kikamilifu na huduma za intaneti za kibiashara, na hivyo kusaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za elimu, biashara, mawasiliano na huduma nyingine za kijamii kupitia teknolojia.

Leave a comment