
Na Mohamed Zongo
Kikosi cha Polisi Reli Tanzania kimeendelea kushirikiana na jamii inayofanya shughuli zake katika ushoroba wa reli kwa kufanya usafi wa pamoja na mafundi wa magari, wauzaji wa chakula maarufu kama mama ntilie, maafisa usafirishaji pamoja na wafanyabiashara ndogondogo katika eneo la Pentagon, Mivinjeni, Kata ya Kurasini, Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, Afisa Mnadhimu wa Kikosi cha Polisi Reli Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mushana Mujema, kwa niaba ya Kamanda wa Kikosi hicho, ACP Matride Kuyeto, amewataka wananchi wa maeneo hayo kuendelea kufanya usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

ACP Mujema amewataka wananchi hao kuwa mabalozi wema katika kulinda na kutunza miundombinu ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa kuwa maeneo wanayofanyia shughuli zao yamezungukwa na miundombinu hiyo.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuitunza amani ya nchi, akieleza kuwa wanaweza kufanya shughuli zao kwa utulivu kutokana na kuwepo kwa amani. Hivyo, amewataka kuendelea kuilinda amani hiyo kwa hali na mali.
Wakati huohuo, Afisa Polisi Jamii wa Kikosi cha Polisi Reli Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Batseba Kasanga, ametoa elimu ya usalama wa reli kwa wananchi wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo la Mivinjeni, akiwataka kutoweka kitu cha aina yoyote kwenye njia ya reli, kwani kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha usalama wa usafiri wa reli.
Kwa upande wake, Kiongozi wa mafundi katika eneo hilo, Joseph Mwamanda, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zake za kuwa karibu na jamii na kusisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kukabiliana na uhalifu.


Leave a comment