
Na Andrea Mbona, Haydom, Mbulu
Wahitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Haydom, mkoani Manyara, wametakiwa kutojiunga na makundi ya kihalifu na makundi rika ya mitaani yanayojihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kuwa yatasababisha kuathiri ndoto zao za maisha.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Msaidizi cha Haydom, Mkaguzi Alex Malimbwi, wakati akitoa nasaha kwa wahitimu hao baada ya kuhitimu elimu ya msingi.
Malimbwi alisema makundi rika ya mitaani yanaweza kuwa chanzo cha matukio mbalimbali ya kihalifu katika jamii, hivyo kuwasa wahitimu hao kuwa makini na marafiki wanaochagua ili kuepuka mazingira yanayoweza kuwapeleka kwenye vitendo vya uhalifu.
“Ninatamani mtambue kuwa uhalifu hauna nafasi katika jamii na endapo mtajiingiza katika vitendo hivyo mtaua ndoto zenu, ikiwemo kutoendelea na masomo,” alisema Malimbwi.
Aidha, alisema wazazi na walezi wana wajibu wa kuwafundisha, kuwaongoza na kuwalinda watoto wanaporejea majumbani, huku akiwataka kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za kijamii na uzalishaji, ikiwemo kilimo na ufugaji.
Alisema ushiriki wa watoto katika shughuli hizo unaweza kuwajenga katika misingi ya uwajibikaji hivyo kupunguza muda wa kujihusisha na makundi au matukio ya kihalifu.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake, Marselina Bahha alishukuru kwa nasaha hizo, akisema zitawasaidia kutambua wajibu wao katika jamii na kuendelea kufuata njia sahihi wanapoanza hatua nyingine ya maisha.

“Tunashukuru kwa nasaha zako, tunaamini zitatukumbusha wajibu wetu katika jamii ili kuhakikisha tunakuwa raia wema na wanaokubalika baada ya kuhitimu masomo ya elimu ya msingi,” alisema Marselina.
Kwa upande wake, mzazi Paskali Lohay alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu kwa jamii na kuomba liendelee kutoa elimu kuhusu madhara ya uhalifu kwa makundi mbalimbali, hususan watoto na vijana.
Alisema elimu hiyo ni muhimu katika kusaidia kujenga jamii inayozingatia amani, upendo, uwajibikaji na maendeleo.
Leave a comment