
Na George Gabriel
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Edward Magala, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliowekwa katika mkataba.
Magala alitoa agizo hilo hivi karibuni wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo katika ziara iliyohudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na Timu ya Menejimenti ya Halmashauri.
Alisema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, hivyo mkandarasi anapaswa kuongeza nguvu kazi, vifaa na muda wa kufanya kazi ili kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Magala aliiagiza kampuni ya SARO Builders Limited, inayotekeleza awamu ya kwanza ya mradi huo, kuzingatia masharti ya mkataba uliosainiwa Aprili 27, 2026, pamoja na kuhakikisha kazi zote zinatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Ibrahimu Mwanauta, alisema Halmashauri itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha mkandarasi anazingatia masharti ya mkataba, ubora wa kazi na muda uliopangwa.
Alisema uongozi wa Halmashauri umejipanga kuhakikisha changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa mradi zinatatuliwa kwa wakati, akisisitiza kuwa ujenzi wa jengo hilo ni muhimu katika kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za kiutawala kwa wananchi wa Nanyumbu.
Mradi wa ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu una thamani ya Shilingi bilioni 3.6, ambapo Serikali Kuu tayari imetoa Sh bilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo.

Leave a comment