Na Mwandishi Wetu, China

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, amewataka wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza nchini Tanzania katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.

Dkt. Chaya alitoa wito huo jana nchini China, ambako yupo katika ziara ya kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.

Katika ziara hiyo, aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, na walitembelea kiwanda cha Yiling Pharmaceutical Company Limited, ambako walijionea teknolojia na mifumo mbalimbali ya kisasa inayotumika katika uzalishaji wa dawa.

Dkt. Chaya alisema Tanzania ina mazingira wezeshi na rafiki kwa uwekezaji wa muda mrefu, huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Alisema uwekezaji katika uzalishaji wa dawa nchini utaimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, sambamba na kuongeza ajira, ujuzi, teknolojia na fursa za biashara kwa Watanzania.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Tanzania kutumia diplomasia ya uwekezaji kuvutia mitaji na teknolojia kutoka China, ikiwa ni hatua inayolenga kukuza uzalishaji wa ndani na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Posted in

Leave a comment