
Na Abel Mwakingwe
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imetakiwa kuhakikisha mifumo ya kidijitali inayotumika katika ufundishaji na ujifunzaji inawafikia walimu na wanafunzi bila vikwazo, ili kuwawezesha kutumia teknolojia hiyo kuongeza ufanisi katika elimu.
Rai hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, wakati wa ziara ya kamati hiyo katika makao makuu ya TET jijini Dar es Salaam.
Sekiboko aliipongeza TET kwa kuendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia na kuandaa mifumo mbalimbali inayosaidia utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa ambao umeanza kutumika nchini tangu mwaka 2024.
Alisema matumizi ya teknolojia katika elimu yanaweza kuongeza ufanisi wa walimu na kuwapa wanafunzi fursa pana ya kupata nyenzo za kujifunzia, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha mifumo hiyo inapatikana kwa urahisi na kutumika ipasavyo.
Aidha, alisema Kamati itaishauri Serikali kushirikiana na kampuni za mawasiliano kutafuta namna ya kupunguza au kuondoa gharama za vifurushi vya intaneti vinavyotumika katika mifumo ya elimu.
alisema hatua hiyo itasaidia walimu na wanafunzi kutumia mifumo hiyo kwa urahisi na kuongeza tija katika ufundishaji na ujifunzaji.
Hatua hiyo inaendana na jitihada za TET za kuendeleza madarasa ya kidijitali ambayo yamekuwa yakitumika katika mafunzo ya walimu na kuunganisha vituo vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ameishukuru Kamati kwa maoni na ushauri uliotolewa kuhusu namna ya kuboresha sekta ya elimu.
Alisema Wizara itafanyia kazi maeneo yaliyoainishwa na Kamati kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizobainishwa na kuendelea kuboresha utoaji wa elimu nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, mafanikio na mahitaji ya taasisi hiyo, akisema TET imeendelea kuweka msisitizo katika matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.
Alisema miongoni mwa mifumo inayotumiwa na taasisi hiyo ni Maktaba Mtandao, inayowezesha upatikanaji wa vitabu kwa njia ya kidijitali, pamoja na Open Public School (OpSchool), mfumo wa udhibiti ubora na Learning Management System (LMS).
Aliongeza kusema mifumo hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa nyenzo za elimu na kurahisisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu na wanafunzi.
Ziara hiyo imefanyika wakati Serikali ikiendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika elimu, ikiwa ni sehemu ya hatua za kukabiliana na mahitaji yanayobadilika katika ufundishaji na ujifunzaji.


Leave a comment